Elizabeth Michael 'Lulu'
Kizaa zaa cha umri wa Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayekabiliwa na kesi inayomhusisha na kifo cha Steven Charles Kanumba kimezidi kushika kasi baada ya baba yake mzazi, Michael Edward Kimemeta kutofautiana na mama mzazi wa Lulu, Lucresia Karugila na kuweka watu njia panda ni nani mkweli na nani si mkweli.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, baba huyo mzazi wa Lulu anayeishi Moshi mkoani Kilimanjaro ambaye hakuwahi kusikika kwenye vyombo vya habari, alijitokeza kwa mara ya kwanza na kudai kuwa binti yake ana umri wa miaka 16.

Baba mzazi wa Lulu, Michael Edward Kimemeta
Baba Lulu alikaririwa akisema: “Mwanangu alizaliwa mwaka 1995, atatimiza umri wa miaka 17 ifikapo Aprili 17, mwaka huu (kesho). Kwa sasa ana umri wa miaka 16.”
Elizabeth 'Lulu' mwenyewe siku alipopandishwa mahakamani alikana ya kuwa ana umri wa miaka 18, na alisema “Mheshimiwa hakimu, naomba kurekebisha umri wangu, nina miaka 17 na siyo 18.” Lulu aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alipofikishwa mahakamani hapo Aprili 11, mwaka huu.
Kwa upande wa mama mzazi wa Lulu alikuwa na haya ya kusema “Mimi ndiye niliyemzaa Lulu, ana miaka 17,” alisema hayo bila kutaja tarehe aliyozaliwa mwanaye kama alivyofanya baba.

Mama mzazi wa Lulu
Naye Mbunge wa Kawe kwa tiketi ya Chadema, Mheshima Halima Mdee alipokwenda Kituo cha Polisi Oysterbay kumuona Lulu, alidai kuwa aliona cheti cha kuzaliwa cha Lulu na kusema: “Niliona cheti cha kuzaliwa, Lulu ana miaka 17,” Mdee aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.
Kwa hiyo mpaka sasa umri wa Lulu umekuwa ni kitendawili na kusababisha kizaa zaa miongoni mwa baadhi ya watu ambao wanataka kujua nini hatma ya staa huyo filamu anayeshukiwa kuhusika na kifo cha aliykuwa gwiji wa filamu nchini Tanzania Steven Kanumba.
No comments:
Post a Comment