Saturday, 14 April 2012

Mrembo kupandishwa mahakamani kwa kutaka kujiua kwa sababu ya kifo cha Kanumba


Mariam Elias (Picha kwa hisani ya Millardayo.com)

Polisi mkoani Pwani inatarajia kumfikisha mahakamani wakati wowote mkazi wa Misugusugu wilayani Kibaha Mariam Elias (19) akituhumiwa kutaka kujiua kwa kukusudia.

Mariam inadaiwa alitaka kujiua kwa kunywa sumu ya panya kwa kile alichokielezea mwenyewe kuwa ni masikitikio yake kutokana na kifo cha msanii maarufu wa filamu nchini Steven Kanumba aliyefariki wiki iliyopita na kuzikwa juzi jijini Dar es Salaam Jumanne.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alisema taarifa za binti huyo kutaka kujiua wamezipata na kwa kuwa bado yupo hospitalini Tumbi akiendelea na matibabu amewekwa chini ya ulinzi.

“Ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai mtu ukitaka kujiua na huyu Mariam alichofanya ni kujaribu kujiua, tumemuweka chini ya ulinzi na tutamfikisha mahakamani wakati wowote akitoka hospitalini,” alisema Kamanda Mangu.

Binti huyo alikaririwa na vyombo vya habari jana kuwa aliomba Sh 200 kwa rafiki yake na kwenda kununua sumu ya panya na kuinywa kutokana na majonzi makubwa aliyonayo kwa kifo cha Kanumba na kwamba kifo hicho kimemuumiza kiasi cha kuona bora anywe sumu ili aondoke duniani amfuate Kanumba huko aliko kutokana na mapenzi aliyonayo kwa kazi zake za filamu.

Hata hivyo, jaribio lake halikufanikiwa kwani alikimbizwa Hospitali ya Tumbi ambako anaendelea na matibabu.

Naye Anastazia Anyimike anaripoti kuwa mama mzazi wa Kanumba amewashukuru Watanzania, viongozi wa Serikali na wapenzi wa mwanawe kwa kujitokeza kumzika mtoto wake.

Kanumba aliyefariki siku ya kuamkia Jumamosi alizikwa Jumanne Makaburi ya Kinondoni, ambapo Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam juzi kwa tuhuma za mauaji ya msanii huyo.

Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu Sinza, mama mzazi wa msanii huyo Flora Mtegoa alisema upendo waliouonesha Watanzania wakati wa msiba wa mwanawe hana cha kuwalipa zaidi ya kuwashukuru.

Chanzo: Habari leo

No comments:

Post a Comment