Thursday, 29 December 2011

Chuo Kikuu cha Zanzibar chakubaliana na chuo kikuu cha Indiana cha Marekani



Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) pamoja na Chuo Kikuu cha Marekani cha Indiana, vimetiliana saini makubaliano ya kuimarisha na kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni Zanzibar.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika chuo hicho kati ya Makamu Mkuu wa Suza, Profesa Idrissa Ahmed Rai na Mkuu wa Kitivo cha Kiswahili cha Chuo Kikuu cha Indiana cha Marekani,
Alawia Omar.

Professa Rai alisema mikakati ya SUZA ni kuhakikisha kwamba Kiswahili kinaongeza wigo wa
kufundishwa kwa watu mbalimbali.

“Tumefurahishwa na mipango ya ushirikiano katika kuimarisha Kiswahili kwa kukifundisha kwa watu wa mataifa mbalimbali ulimwenguni,” alisema.

Alisema mikakati ya kukipanua Kiswahili inakwenda sambamba na mipango ya viongozi wa
Umoja wa Afrika wa kutaka lugha hiyo sasa kutumiwa katika taasisi na vyombo mbalimbali vikiwemo vya kutunga sheria.

Naye Alawia alitoa vifaa mbalimbali vya kufundishia Kiswahili kwa ajili ya matumizi ya Suza.

No comments:

Post a Comment